Thursday, March 14, 2013

Msindai awataka wachimbaji madini wa Nkokilangi – Singida kuwa wavumulivu wakisubiri utatuzi wa mgogoro wao.

 Mwenyekiti wa CCM mkoa wa Singida Mgana Msindai (wa kwanza kulia) akizungumza na wachimbaji wa dhahabu katika mgodi wa kijiji cha Nkokilangi wilaya ya Iramba mkoani Singida.
Mwenyekiti wa CCM mkoa wa Singida Mgana Msindai (katikati) akiangalia shimo la kuchimba madini aina ya dhahabu katika kijiji cha Nkokilangi tarafa ya Shelui wilaya ya Iramba. Wa kwanza kushoto ni Katibu Msasidizi CCM mkoa wa Singida Ndembo na kulia ni mmiliki wa shimo hilo Bw. Omari.

Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) mkoa wa Singida Mgana Msindai amewataka wachimbaji dhahabu katika machimbo ya Nkokilangi wilaya ya Iramba, kuwa wavumilivu kipindi hiki ambacho mgogoro kati yao na wachimbaji wenye leseni ukitafutiwa ufumbuzi wa kudumu.
Msindai ametoa rai hiyo wakati akizungumza na baadhi ya wachimbaji dhahabu wa kijiji cha Nkokilangi na maeneo jirani.
Amewataka wajiepushe kabisa na hasira na badala yake wawe wavumilivu na kutii sheria zikiwemo zinazotawala sekta ya madini.
 “Wahenga waliishasema kwamba hasira ni hasara na pia mambo mazuri siku zote hayahitaji haraka”.
Kuweni wavumilivu, jiepusheni na uchochezi wa aina yo yote na msithubutu kabisa  kujichukulia sheria mikononi mwenu, mkifanya hivyo sheria itachukua mkondo wake”,alisema mwenyekiti huyo wa mkoa.
Msindai amesema CCM mkoa inaufahamu vema mgogoro wa wachimbaji dhahabu wa Nkokilangi  wasiokuwa na leseni na wale wenye leseni, ambao umedumu kwa muda sasa.
 “CCM siku zote inataka kuona Watanzania wakiwemo wachimbaji wa madini wanafanya shughuli zao kwa amani na utulivu mkubwa.
Kutokana na ukweli huo, kamati ya siasa mkoa wa Singida, imeelekeza nguvu zake kutafuta njia sahihi ya kutafuta ufumbuzi wa kudumu.
Wachimbaji wenye leseni wachimbe kwa amani katika maeneo yao na wasio na leseni wajitahidi wapate”,amefafanua Msindai.
Wachimbaji wengi wa dhahabu katika machimbo ya Nkokilangi kwa miaka mingi wamekuwa wakifanya shughuli zao bila kuwa na leseni.
Baada ya hivi karibuni baadhi ya wachimbaji kumiliki maeneo mengi kwa kuwa na leseni halali ,ndipo kulikopelekea mgogoro mkubwa kuibuka.

No comments:

Post a Comment