Tuesday, March 19, 2013

TANROADS Singida yatumia zaidi ya sh. Bilioni 2.2 kutengezeka barabara na madaraja 14 kwa kipindi cha Julai ’12 hadi Februari’13.

 Meneja wa TANROADS mkoa wa Singida mhandisi Yustaki Kangole, akitoa taarifa yake kwenye kiako cha bodi ya barabara mkoa wa Singida kilichofanyika katika ukumbi wa mikutano wa ofisi ya mkuu wa mkoa mjini Singida.
Mkurugenzi wa halmashauri ya manispaa ya Singida Mathias Mwangu,akichangia maoni  kwenye kikao cha 34 cha bodi ya barabara mkoa wa Singida kilichofanyika katika ukumbi wa mikutano wa ofisi ya mkuu wa mkoa wa Singida mjini Singida.

Wakala wa barabara (TANROADS) mkoa wa Singida, umetumia zaidi ya sh. 2.2 bilioni kugharamia matengenezo mbalimbali ya barabara zake na madaraja 14, kwa kipindi cha kuanzia Julai mwaka jana hadi Februari mwaka huu.
Akitoa taarifa yake mbele ya kikao cha 34 cha bodi ya barabara, kilichofanyika kwenye ukumbi wa mikutano wa ofisi ya mkuu wa mkoa mjini Singida, Meneja wa TANROADS mkoa wa Singida Mhandisi Yustaki Kangole, amesema baadhi ya fedha hizo, Sh. 301.6 milioni, zimetumika kugharamia
matengenezo ya kawaida ya kilomita 134.1 ya barabara kuu, wakati shs. 374.6 milioni zimetengeneza kilomita 361 za barabara za mkoa.
Mhandisi Kangole amesema matengenezo ya vipindi maalum yamefanyika katika barabara za Manyoni mjini na Rungwa – Itigi – Mkiwa ambayo kilomita 16.6 zimetengenezwa kwa gharama ya zaidi ya shs. 238.8.
Kuhusu sehemu korofi, meneja huyo  amesema kilomita 15.3 katika barabara za mkoa, zimetengenezwa kwa gharama ya zaidi Shs.184.6 milioni.
Aidha, Kangole amesema jumla ya madaraja matano makubwa, yanafanyiwa matengenezo kwa gharama ya zaidi ya shs. 534.1 milioni, wakati madaraja madogo tisa yametengenezwa kwa zaidi ya shi. 38.2 milioni.
Mhandisi Kangole amesema fedha zilizotumika hadi mwishoni mwa Februari ni sawa na asilimia 25 ya kiasi kilichoidhinishwa kwa mwaka wa fedha wa 2012/2013 cha zaidi ya Sh. 9 bilioni.
Wakati huo huo, kikao hicho kilichokuwa chini ya uenyekiti wa mkuu wa mkoa wa Singida Dk.Kone, kilipitisha kwa kauli moja kwamba kuanzia sasa katibu wa kikao hicho atakuwa meneja wa TANROADS mkoa badala ya katibu tawala ambaye imedaiwa kukabiliwa na majukumu mengi.
Wakala wa barabara mkoa wa Singida, unahudumia jumla ya kilomita 1,689.5 za barabara kuu na barabara  za mkoa. 
Kati ya hizo, kilomita 367.9 ni za lami ambayo ni sawa na asilimia 21.8, wakati sehemu iliyobaki yenye kilometa 1,321.6 sawa na asilimia 78.2 ni barabara za changarawe/udongo.

No comments:

Post a Comment