Wednesday, March 13, 2013

wachimbaji wadogo wapewa mafunzo singida.

Veronica Francis, Mjiolojia Wizara ya nishati na madini akifafanua jambo kwenye mafunzo kwa wachimbaji wadogo wa machimbo ya dhahabu.
Katika picha ya pamoja washiriki wa mafunzo ya uchimbaji madini machimbo ya Sambaru mkoani Singida

WACHIMBAJI wadogo wametakiwa kufanya kazi zao za uchimbaji madini kwa kufuata sheria, kanuni na taratibu, ili kuepuka uharibifu wa mazingira unaotokana na ukataji miti na matumizi ya kemikali kwenye migodi.


Wito huo ulitolewa na Mkuu wa wilaya ya Ikungi mkoani Singida Manju Msambya wakati akifungua mafunzo ya siku tano kwa wachimbaji wadogo wa dhahabu wa machimbo ya Sambaru wilayani humo na Londoni katika wilaya Manyoni mkoani Singida.
Msambya alisema kuwa, kukithiri kwa uchafuzi wa mazingira unaotokana na zebaki kwa ajili ya kukamatisha dhahabu hauzingatii wala kufuata teknolojia safi na salama kwa kazi hiyo inayowaingizia
kipato kwa ajili ya familia zao.
"Hapa Sambaru kumekithiri uchafuzi wa mazingira kwa kutumia zebaki....matumizi haya yasiyozingatia teknolojia safi na salama yanahatarisha maisha ya watu, mimea na mifugo hasa kwa kuzingatia uchafuzi huu unafanyika kwenye mabonde,"alisema Msambya.

Kwa upande wake kamishina msaidizi wa madini kanda ya kati, Manase Mbasha alisema mafunzo hayo ni ya kwanza kufanyika nchini, yakienda sambamba na yale yanayotolewa hivi sasa katika eneo la Mugusu, mkoani Shinyanga.
Alisema anaamini baada ya wachimbaji kupata mafunzo hayo, watabadilika na kuanza kuboresha kazi zao kwa ufanisi zaidi.
Naye mjiolojia kutoka wizara ya nishati na madini, inayosimamia mafunzo hayo, Veronica Francis Nangale alisema baada ya elimu hiyo, anaamini wachimbaji watayaelewa vema mazingira yanayowazunguka na hivyo kunufaika zaidi kiuchumi.
Alisema mada mbalimbali za uchimbaji madini zinatolewa na wataalamu kutoka wizarani na chuo kikuuu cha Dar es Salaam (UDSM), ikiwemo kutengeneza migodi kwa ufasaha, Ujasiriamali, maytumizi ya vifaa vya kuchimbia na Ukimwi, ili kuongeza uzalishaji wa kazai zao.

Aidha baadhi ya washiriki wawili kati ya 38 wanaohudhuria mafunzo hayo ya siku tano, akiwemo Agnetha Edwin na Paulo Msalaba walisema wanaamini baada ya mafunzo hayo, wataboresha kazi zao na kuzalisha zaidi, huku pia wakitoa wito kwa serikali kuendesha mafunzo kama hayo mara kwa mara.

No comments:

Post a Comment