Kamanda wa jeshi la polisi
mkoa wa Singida Linus Sinzumwa (kushoto) akishikilia silaha ya kijeshi
bunduki aina ya SMG aliyodai kukamatwa ikiwa imehifadhiwa ndani ya
sanduku la nguo na kufichwa kwenye shamba la mahindi katika kijiji cha
Itigi jimbo la Manyoni Magharibi. Bunduki hiyo inadhaniwa kuwa ilikuwa
ikitumika kwenye matukio ya uhalifu ikiwemo ujambazi. Juu ya meza ni
risasi 30 za SMG hiyo. Kulia ni afisa upelelezi (RCO) wa makosa ya jinai
mkoa wa Singida Thobias Sedoyeka.
Jeshi
la polisi mkoani Singida limefanikiwa kukamata silaha ya kijeshi
bunduki aina ya SMG na risasi zake 30, ambayo inadhaniwa kuwa ilikuwa
ikitumika katika matukio ya uhalifu mbalimbali ukiwemo wa ujambazi wa
kutumia silaha.
Akizungumza
na waandishi wa habari ofisini kwake, Kamanda wa polisi mkoa wa Singida
Linus Sinzumwa, amesema kuwa bunduki aina ya SMG waliyoikamata ina
namba za usajili UA 39621992 na imekamatwa Machi tano mwaka huu, kwenye
msako mkali unaoendelea mkoani Singida kusaka wahalifu mbalimbali.
Amesema
kuwa mtu mmoja amekamatwa kwa
tuhuma ya kumiliki bunduki hiyo ya
kijeshi kinyume cha sheria na kwamba kwa sasa, jina la mtuhumiwa
haliwezi kutangazwa kwa vile vinaweza kuharibu upelelezi unaoendelea.
Sinzumwa
amesema kuwa silaha hiyo, ilikamatwa ikiwa imehifadhiwa ndani ya
sanduku la nguo ambalo lilifunikwa na majani na kuwekwa katikati ya
shamba la mahindi.
Amesema
mafanikio hayo makubwa yametokana na ushirikiano mkubwa uliotolewa na
raia wema ambao walitoa taarifa sahihi zilizoweza kusaidia mtuhumiwa
kukamatwa pamoja na silaha hii ya kijeshi na kuwaomba wananchi waendelee
na moyo huo huo wa kutoa ushirikiano ili kusaidia vita hivi vya
kukomesha vitendo vya uhalifu mkoani Singida.
Aidha amesema uchunguzi/upelelezi ukikamilika, mtuhumiwa atafikishwa mahakamani kujibu tuhuma inayomkabili.
Katika
tukio jingine, Kamanda Sinzumwa amesema huko katika mtaa wa Karakana
mjini Singida, Tatu Idd (25) alikamatwa akimiliki lita tano za pombe
haramu ya gongo pamoja na mtambo wake.
“Pia
siku hiyo hiyo, Abbakari Mohammed (30) tumemkamata akiwa na misokoto ya
bangi 15 ndani ya mifuko yake ya suruali ambayo alikuwa akiitembeza
kuiuza. Vijana wanane ambao tunahisi kuwa ni vibaka sugu nao
tumewakamata tunaendelea kuwahoji. Muuza gongo sugu Tatu, muuza bangi
Abbakari na vibaka nane, tukimaliza upelelezi, tunatarajia kuwafikisha
mahakamani kujibu tuhuma zinazowakabili”, amesema.
No comments:
Post a Comment