Thursday, January 9, 2014

Wakazi wa kijiji alikozaliwa IGP Mangu wapokea uteuzi wa mwana wao kwa bashasha.

Mama mzazi wa IGP Ernest Mangu,mkazi wa kijiji cha Kihanuda tarafa ya Ilongero wilaya ya Singida, Bi. Mwanaidi Msengi akipasua kuni  kwa ajili ya kupikia chakula.
Mama mzazi wa IGP, Ernest Mangumkazi wa kijiji cha Kihanuda tarafa ya Ilongero wilaya ya Singida,akiwa amejitwisha chungu akiwa nyumbani kwake.Mama huyo,amedai kuwa alifanya biashara ya kuuza vyumba na kupata fedha za kugharamia masomo ya Mangu.
Makazi ya wazazi wa IGP Ernest Mangu yaliyoko katika kijiji cha Kihanuda tarafa ya Ilongero wilaya ya Singida.
Rais Jakaya Mrisho Kikwete akimwapisha Inspekta Generali wa Polisi (IGP) mpya Afande Ernest Mangu katika viwanja vya Ikulu jijini Dar es salaam.

UTEUZI  wa Mkuu Mpya wa Jeshi la Polisi nchini (IGP) Kamishna Ernest Mangu umepokelewa kwa nderemo, vifijo na bashasha na wakazi wa kijiji cha Kihunadi tarafa ya Ilongero wilaya na mkoa wa Singida alikozaliwa IGP huyo kwa madai kwamba sasa kijiji chao kitajulikana haraka ndani na nje ya Tanzania.

Wamedai pamoja na faida ya kujulikana huko,changamoto mbali zinazokikabili kijiji hicho zitapatiwa ufumbuzi wa kudumu mapema iwezekanavyo.

Wamedai zaidi kwamba wamekuwa wakiamini kwa Kamishna Mangu atafika mbali katika kushika nafasi za juu za uongozi kutokana na uadilifu, uchapaji kazi, ukaribu wake kwa wananchi, uaminifu na uwazi wake.

Kwa upande wa mama yake mzazi Mwanaidi Msengi, pamoja na furaha kubwa aliyonayo, amemwasa mtoto wake huyo kuchapa kazi kwa bidii kama njia mojawapo ya kumshukuru Rais Kikwete kwa kumteua kuwa mzawa wa kwanza wa mkoa wa Singida, kushika wadhifa huo nyeti.

“Hii ni heshima kubwa sana kwangu binafsi, ndugu zake, wakazi wa kijiji cha Kihunadi na mkoa wa Singida, kwa hiyo lengo langu ni kumwombea mtoto wangu Mangu asimwangushe Rais, atimize wajibu wake ipasavyo ili Rais Kikwete siku moja aseme hajakosea kumpa Mangu, ukuu wa polisi nchini”,amesema kwa kujiamini.

Mwanaidi amesema Mangu alianza elimu ya msingi katika shule ya Kinyagigi, alikuwa na bidii mno katika kujisomea.  Kwenye mitihani mara nyingi alishika nafasi ya kwanza au  ya pili, akifanya vibaya alishika nafasi ya tatu.

“Mwaka 1977 alifaulu mtihani wa darasa la saba na kuchaguliwa kujiunga na elimu ya sekondari katika shule ya Tumaini iliyopo Kinampanda wilayani Iramba aliyomaliza kidato cha nne”,amesema.

Akifafanua, Mwanaidi amesema alipofaulu kujiunga na elimu ya sekondari, alilazimika kuomba ng’ombe kwa mke mweza, ili akamuuze apate fedha za kugharamia masomo ya mtoto wake.

“Nadhani mke mwenzangu huyo, alimtoa ng’ombe wake kwa shingo upande kwa sababu Mangu alipomuuza kwenye mnada pale Singida mjini, aliibiwa fedha zote na alirudi nyumbani akilia sana”,amesema.

Amesema baada ya hapo, alimwambia mtoto wake Mangu, kwamba hawataomba tena ng’ombe na badala yake atatengeneza vyungu kwa kutumia udongo wa mfinyanzi  ili kupata fedha za kugharamia masomo yake.

“Nashukuru Mangu alinielewa vizuri kwa sababu alishiriki kubeba kichwani vyungu hivyo wakati wa kuviuza hadi kichwa chake kilikaribia kuwa kipara.  Nilibuni chanzo kingine cha mapato ambacho kilikuwa ni kukoroga na kuuza

pombe”,amesema.

Kwa mujibu wa Mwanaidi, Kamishna Mangu ni mtoto wa pili kati ya watoto saba, aliowazaa.

Aidha,Mwanaidi ni kati ya wake sita waliowahi kuolewa na baba yake Kamishna Mangu, Jumbe Omari Mangu, aliyefariki aprili 27 mwaka 1988.  Jina la Jumbe linatokana na kupewa kazi ya ujumbe wa wakoloni wakati wa ujana wake.

Inadaiwa kwamba baba yake Kamishina Mangu, alioa wanawake hao sita, kwa nyakati tofauti kwa lengo la kusaka mtoto/watoto wa kiume.  Wengi wa wake hao, walikuwa wanazaa watoto wa kike.

No comments:

Post a Comment