Wednesday, January 8, 2014

Halmashauri ya Ikungi kutumia shilling 512.3milioni kwenye miradi ya maendeleo.

Mkurugenzi mtendaji wa halmashauri ya wilaya ya Ikungi, Protace Magayaye, akitoa taarifa yake kwa waandishi wa habari (hawapo kwenye picha)  ya utekelezaji wa shughuli za kilimo msimu wa 2013/2014 ambapo wanatarajia kuvuna tani 144,826 mazao ya chakula na hivyo kuwa na ziada tani 83,090.Mahitaji ya wakazi wa wilaya hiyo 225,521,ni tani 61,736 kwa mwaka.

HALMASHAURI ya Wilaya ya Ikungi Mkoani Singida inatarajia kutumia zaidi ya shilingi 512.3 milioni kugharamia miradi mbalimbali ya maendeleo ya wananchi katika kipindi cha mwaka wa fedha wa 2013/2014.
Fedha hizo zimepokelewa na Halmashauri hiyo hadi kufikia mwezi huu wa Desemba mwaka huu.

Hayo yamesemwa na Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri hiyo, Protace Magayane wakati akizungumza na moja ya magazeti ya kila siku ofisini kwake juu ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo ya wananchi.
Alitaja baadhi ya miradi ya maendeleo wanayoitekeleza kuwa ni ujenzi wa hostel katika shule ya sekondari Ikungi ujenzi wa nyumba ya watumishi ya kijiji cha Kimbwi na kuboresha mazingira ya kujifunzia kwa watoto wenye mahitaji maalum wa shule ya msingi Ikungi.

Magayane alitaja miradi mingine kuwa ni kuendesha mafunzo ya mashamba darasani kwa wakulima 10 na ununuzi wa mbegu bora, ukarabati wa tanki la maji Iyumbu na matengenezo ya barabara za vijiji vya Mungaa-Ntuntu,Utaho-Makiungu na Ikungi- Ndung’unyi.
Katika hatua nyingine, Mkurugenzi huyo alitaja baadhi ya mikakati ya kuboresha utekelezaji miradi kuwa ni uongozi wa Halmashauri kwa kushirikiana na wadau wa maendeleo kuendelea kuzihamasisha jamii kushiriki kuchangia, kutunza na kumiliki miradi yao.

“Kuhakikisha vijiji na kata zinatoa taarifa za
mapato na matumizi kila mwezi/robo mwaka ili kuwapa wananchi moyo wa kuchangia katika miradi husika na kubuni vyanzo vipya vya mapato na kuhakikisha mapato ya ndani yanaongezeka kwa mwaka wa fedha wa 2014/2015″,amesema Magayane.


No comments:

Post a Comment