Meneja wa mikopo wa SIDO mkoa wa Singida, Ruben Mwanja akiwa ofisini kwake akiwajibika katika majukumu yake ya kila siku.
Jengo la ofisi ya SIDO mkoa wa Singida iliyopo Utemini mjini Singida.
SHIRIKA la kuhudumia viwanda vidogo (SIDO) mkoani Singida limetoa mikopo mbali mbali yenye thamani ya zaidi ya shilingi 966.1 milioni kwa wafanyabiashara 1,326, katika kipindi cha mwaka jana.
Hayo yamesemwa hivi karibuni na Meneja Mikopo wa SIDO mkoa wa Singida, Reben Mwanja wakati akizungumza na Mwandishi wa habari hizi ofisini kwake, juu ya maendeleo ya utoaji wa mikopo kwa wafanyabiashara wadogo.
Amesema kati ya fedha hizo, shilingi 457,000,000 zilitolewa kwa wakopaji/wanachama 1,0104 wa vikundi vya (solidality group), VICOBA na benki za jamii vijijini na vikundi hivyo vilikuwa 45.
“Pia shilingi 509,150,000/= zilitolewa kwa wakopaji mmoja mmoja wapatao 312. Mikopo hiyo, lengo lake ni kuwaendeleza wafanyabiashara wadogo wadogo na wa kati na sekta ya viwanda”,amesema Mwanja kwa kujiamini.
Akifafanua zaidi, Mwanja amesema kuwa kati ya wateja 1,326 walionufaika na mikopo hiyo mwaka jana, wanawake walikuwa 717 na wanaume ni 609.
Aidha,meneja huyo amesema mikopo hiyo ilitolewa katika wilaya zote za mkoa wa Singida na kwamba imewanufaisha wafanyabiashara wadogo,viwanda, uvuvi, ufugaji na wachimbaji wadogo wadogo.
Kuhusu marejesho,Mwanja amesema kuwa marejesho ya mikopo ni asilimia 98 na kwa ujumla,hayasumbui wakopaji wanarudisha bila shida kubwa.
“Marejesho hayo mazuri, yanachangiwa kwa kiwango kikubwa na utoaji mafunzo kabla mhusika hajapewa mkopo, na vile vile usimamizi wa karibu na uendeshaji wa biashara”,amesema Mwanja.
Wakati huo huo, Meneja Mwanja amewashauri
wananchi wa mkoa wa Singida kujiunga kwenye vikundi ili waweze kujijengea mazingira mazuri ya kukopeshwa na SIDO.
Meneja huyo wa mikopo,pia alivishauri vikundi kuangalia uwezekano wa kuanzisha viwanda vidogo vidogo vya kukamua alizeti pamoja na asali kwa maneo ya vijiji vya Isuna, Manyoni na Itigi.
“Naomba nitumie nafasi hii,kuwaomba na kuwasihi wakazi wa mkoa wetu wa Singida,kujiunga katika vikundi ili waweze kujijengea mazingira mazuri ya kukopesheka na taasisi za kifedha kwa urahisi.Sisi SIDO tunavikaribisha sana vikundi kuja kuchukua mikopo kwa ajili ya kujiendeleza na kuinua vipato vyao”,amesema meneja hyuo.
No comments:
Post a Comment