Monday, January 20, 2014

Mtoto aibiwa katika mazingira ya kutatanisha.

Kamanda wa polisi mkoani Singida, SACP Geofrey Kamwela, akizungumza na waandishi wa habari (hawapo pichani) kuhusiana na tukio la kupotea kwa mtoto.

MTOTO Meristina Samwel mwenye umri wa mwezi mmoja na siku moja mkazi wa Misuna Manispaa ya Singida ameibiwa katika mazingira ya kutatanisha.

Kamanda wa polisi mkoani Singida, SACP Geofrey Kamwela amesema tukio hilo la wizi wa mtoto, limetokea Januari 14 mwaka huu saa tano asubuhi huko katika mtaa wa Ginery kata ya Mandewa tarafa ya Unyakumi Manispaa ya Singida.

Amesema siku moja kabla ya tukio, mwanamke ambaye jina lake bado halijafamika, alifika Misuna nyumbani kwa mama wa mtoto aliyeibiwa, aitwaye Fatuma Jumanne (26) na kudai anatafuta mtoto wa kazi.

 “Baada ya mazungumzo ya muda kati ya wanaweke hao, kulijengeka aina fulani ya urafiki uliopelekea mwanamke mwizi wa mtoto kurudi tena  nyumbani kwa Fatuma”,amesema.

Kamwela amesema siku hiyo januari 14 saa tano asubuhi, mwanamke huyo, akiwa nyumbani kwa Fatuma alimwombwa mwenyeji wake waende wote Ginery ili akamwonyeshe nyumbani kwake.

Akifafanua zaidi, amesema kwa vile Fatuma alikuwa na watoto wawili, yule mwanamke mwizi, aliomba kubeba mtoto mchanga na Fatuma akabeba yule mkubwa.

 “Walipofika Ginery, mwanamke mwizi alimpeleka Fatuma mgahawani akamnunulia
chai vitafunwa na soda.  Baada ya kutoa ‘ofa’ hiyo, mwanamke huyo alimwaga Fatuma kuwa anaenda duka jirani kuchukua ufunguo wa nyumba yake huku akiwa na kitoto kichanga”,amesema.

Kamwela amesema mwanamke huyo huku akiwa amembeba Meristina, hakuweza kurudi tena kwa Fatuma na badala yake kupotelea kusikojulikana na mtoto huyo.

Kamanda huyo amesema juhudi za kumtafuta mtoto na mwanamke huyo mwizi zinaendelea na amewataka wananchi kuwa endapo watamtilia  shaka mwanamke mwenye mtoto mchanga watoe taarifa kituo chochote cha polisi.

No comments:

Post a Comment