Thursday, March 21, 2013

Tatizo la uhaba wa maji kwa wakazi wa Singida kumalizika mwishoni kwa mwezi ujao.

Serikali ya mkoa wa Singida imesema tatizo la muda mrefu la uhaba wa maji kwa wakazi wa Singida mjini, litakuwa historia ifikapo mwishoni mwa mwezi ujao, baada ya mradi mkubwa wa maji unaofadhiliwa na benki ya kiarabu (BADEA) na shirika la mafuta ulimwenguni (OPEC) utakapomalizika.
Akizungumza kwenye uzinduzi wa wiki ya maji uliofanyika katika eneo la Irao, halmashauri ya manispaa ya Singida, Mkuu wa mkoa wa Singida Dk.Parseko Vicent Kone akifafanua, amesema kuwa utekelezaji wa mradi huu, umefikia kiwango cha aslimia 93 na unategemewa ifikapo
Aprili 30 mwaka huu, utakuwa umekamilika.
Amesema mwishoni mwa mwezi ujao,maji safi na salama yatakapitana kwa asilimia mia moja, hii ni neema kubwa mno ambayo serikali ya awamu ya nne inawapatia wakazi wa mji wa Singida.
Katika hotuba yake iliyosomwa kwa niaba yake na mkuu wa wilaya ya Singida Mwalimu Queen Mlozi, mkuu huyo wa mkoa amewataka wakazi wa mji wa Singida,kujenga kuwa na mwamko wa kulipa ankara zao za maji, kama njia moja wapo ya kuishukuru serikali kwa kuwaondolea matatizo ya upatikanaji wa maji.
“Pia nawaombeni sana mjenge utamaduni wa kuwafichua watu wanaojiunganishia maji kiholela, , kuchepusha dira za maji na wanaofanya uharibifu wa miundo mbinu ya maji ikiwemo mabomba” amesema.  
Awali Meneja biashara wa mamlaka ya maji safi na usafi wa mazingira Singida mjini (SUWASA), Hosea Maghimbi, alisema madhumuni ya wiki hiyo ya maji ni pamoja na kutoa fursa kwa wananchi kuielewa kikamilifu programu ya maendeleo ya sekta ya maji ili waweze kushiriki utekelezaji wake.
 Alitaja madhumuni mengine kuwa ni kutoa elimu kwa umma kuhusu matumizi bora ya maji, kuwaelimisha wananchi kuhusu utunzaji wa mazingira kwenye vyanzo vya maji na kuwahamasisha wateja wake wa maji katika ulipaji wa ankra za maji kwa wakati na kulipa malimbikizo ya madeni.
Kauli mbiu ya wiki ya maji kwa mwaka huu ni ‘mwaka wa ushirikiano wa maji kimataifa’.

No comments:

Post a Comment