Tuesday, March 5, 2013

Wilaya ya Mkalama mkoani Singida yaomba kupatiwa mamlaka kamili ya halmashauri ili kukidhi maendeleo.

Mkuu wa wilaya mpya ya Mkalama mkoani Singida,Edward Ole Lenga akihimiza shughuli za maendeleo katika mkutano wa hadhara uliofanyika hivi karibuni katika kijiji cha Gumanga kata ya Nduguti.

Serikali ya wilaya ya Mkalama mkoani Singida imeiomba serikali kuu kupitia OWM-TAMISEMI, kuipatia mamlaka kamili ya halmashauri, ili pamoja na mambo mengine, kukidhi haja ya maendeleo kwa wananchi wa wilaya hiyo teule.
 Ombi hilo limetolewa na Mkuu wa wilaya hiyo Edward Ole Lenga, wakati akitoa taarifa yake ya utekelezaji wa ilani ya CCM ya uchaguzi kwa kipindi cha kuanzia mwaka 2005 hadi Desemba mwaka jana.
 Amesema upo umuhimu mkubwa wa uwepo wa Mkurugenzi Mtendaji wa halmashauri na wakuu wa idara mbalimbali, kwa ajili ya kuharakisha upatikanaji wa maendeleo endelevu.
Amesema kutokana na umuhimu huo, kuna haja kubwa kuanzishwa mapema kwa halmashauri itakayokuwa kamili kwa kuwa na Mkurugenzi Mtendaji na wakuu wa idara zote.
 Katika hatua nyingine, Lenga amesema katika kipindi cha kuanzia mwaka 2005/2006 hadi 2011/2012, uzalishaji wa zao la uwele umeongezeka toka tani 0.8 hadi tani 1.5 kwa hekta, mtama toka tani 1.0 hadi tani 1.5 na maharage tani 0.3 hadi tani 0.5 kwa hekta.
 Lenga amesema uzalishaji wa mazao hayo umeiongezeka kutokana na matumizi ya mbolea ya samandi ambayo yameongezeka toka tani 239,658 mwaka 2005/2006 hadi tani 280,000 mwaka 2011/2012.
 Aidha, Mkuu huyo wa wilaya amesema kumekuwa na ongezeko la matumizi ya zana bora za kilimo.
 Amesema takwimu zilizopo zinaonyesha kuwa mwaka 2005 kulikuwa na matrekta 24 na powertiller 4, hadi kufikia juni 2012, idadi ya zana hizi imeongezeka na kufikia matrekta 48 na powertiller 31.
 Kuhusu mipango ya baadaye ya wilaya hiyo, Lenga ametaja baadhi ya mipango hiyo kuwa ni pamoja na kufufua na kuimarisha kilimo cha umwagiliaji ambapo lengo ni kumwagilia ekari 1,000 ifikapo mwaka 2015 na kuimarisha vyama vya ushirika wa mazao, ili wakulima waweze kuuza mazao yao ya biashara kwa faida.

No comments:

Post a Comment