Wednesday, October 30, 2013

Kero za wananchi zinahitaji majadiliano ya pamoja.

Mkurugenzi mtendaji wa halmashauri ya wilaya ya Ikungi, Protace Magayane akizungumza kwenye mahafali ya 13 ya shule ya sekondari Sepuka.
Mkurugenzi mtendaji wa halmashauri ya wilaya ya Ikungi, Protace Magayane (mwenye miwani) akimkabidhi cheti cha kuhitimu kidato cha nne mmoja kati ya 58 wa shule ya sekondari Sepuka.

Baadhi ya wazazi/walezi wa wanafunzi wanaotarajiwa kumaliza kidato cha nne mwaka huu wa shule ya sekondari ya Sepuka wilaya ya Ikungi.

Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Ikungi mkoani Singida Protace Magayane amewahimiza wazazi  na walezi kujenga utamaduni wa kujadili kwa pamoja kero zinazowakabili katika maeneo yao na kuzitafutia ufumbuzi wa kudumu.

Magayane ametoa changamoto hiyo hivi karibuni wakati akizungumza kwenye kilele cha mahafali ya 13 ya shule ya sekondari ya Sepuka, Jimbo la Singida Magharibi.

Akifafanua amesema katika mikutano ya kitongoji, Kijiji na Kata wananchi hawana budi kuweka bayana kero na shida zao na kuzipa vipaumbele.

Akitoa mfano, Magayane amesema katika majadiliano hayo ya pamoja, wanaweza kubainisha kero zinazowakabili katika sekta mbalimbali zikiwemo za sekta ya barabara, maji, elimu na afya.

“Wananchi kwa ushirikiano na viongozi wenu,baada ya kujadiliana,muweke mikakati ya pamoja ya namna ya kutumia nguvu zenu wenyewe katika kutatua kero hizo”,alifafanua Mkurugenzi huyo.

Aidha amewataka katika majadiliano hayo waweke utaratibu wa matumizi bora ya raslimali za ardhi, maliasili, madini na zinginezo ili
ziweze kusaidia kuendeleza maeneo yao.

“Jengeni utamaduni wa kutatua migogoro yenu kwa kutumia haki na busara na wala si kwa kutumia nguvu,” amesema.


Katika mahafali hayo jumla ya wanafunzi 58 kati yao wavulana ni 27 na wasichana ni 31 wamehitimu.

No comments:

Post a Comment