Thursday, October 24, 2013

WALIOISACHI MAITI NA KUFANYA UNYANG'ANYI WAHUKUMIWA MIAKA 120 JELA.

Askari wa polisi mjini Singida akiwaelekeza washitakiwa wanne wa kesi ya unyang’anyi wa kutumia silaha kuingia kwenye gari tayari kwenda kuanza kutumikia adhabu zao kila mmoja miaka 30 jela baada ya kutiwa hatia kwa kosa la unyang’anyi wa kutumia silaha.Washitakiwa hao walitiwa hatiani kwa kosa la kuteka gari la chuo kikuu cha SUA SU 37012 na kisha kuwapora abiria shilingi 8.7 milioni.Pia walibomoa na kusachi  jeneza lililokuwa limehifadhiwa mwili wa marehemu mwanafunzi wa SUA,Munchari Lyoba uliokuwa ukipelekwa mkoa wa Mara kwa mazishi. 
Mshitakiwa aliyetiwa hatiani kwa kosa la unyang’anyi wa kutimia silaha na kupora abiria wa gari la SUA shilingi 8.7 milioni Hamisi Issah (wa kwanza kulia) akipanda gari tayari kwenda kuanza kutumikia adhabu yake jela miaka 30.Pia mwenye kofia ya bakharasia,Abubakari Jumanne naye katiwa hatiani kwa kosa la unyang’anyi.

Washitakiwa wanne waliotiwa hatiani kwa kosa la unyang’anyi wa kutumia silaha wakiwa kwenye gari la polisi tayari kwenda kuanza adahabu zao za kila moja miaka 30.Washitakiwa hao walitiwa hatiani kwa kosa la kuteka gari la chuo kikuu cha SUA na kupora abiria shilingi 8.7 milioni.Washitakiwa hao pia inadaiwa walibomoa jeneza lililokuwa limebeba mwili wa mwanafunzi wa SUA Munchari Lyoba na kulisachi kwa imani kuwa limetumika kuhifadhi mali.

Mahakama  ya wilaya ya Singida imewahukumu vijana wakulima wanne wakazi wa Manispaa ya Singida adhabu ya kutumikia jumla ya miaka 120 jela baada ya kupatikana na hatia ya unyang’anyi wa shilingi 8.7 milioni kwa kutumia silaha.

Washitakiwa hao kabla na baada ya unyang’anyi huo walitumia silaha aina ya bunduki,nondo,mawe na fimbo katika kufanikisha azma yao hiyo.

 Washitakiwa hao vijana ambao kila mmoja atatumikia jela miaka 30,ni Hamisi Ally (23),Hamisi Issa (33),Khalid Hamisi (21) na Abubakari Jumanne (26) wote wakazi wa kijiji cha Kisaki Manispaa ya Singida.

Mshitakiwa  aliyekuwa wa kwanza kwenye kesi hiyo Idd Omari (38) mkazi wa kijiji cha Kisaki aliachiwa huru awali baada ya kutokutambuliwa na walalamikaji katika paredi mbili za utambuzi  zilizofanywa na Jeshi la Polisi.

 Washitakiwa hao pia wanadaiwa kuwa baada ya kufanikiwa kupora mali na fedha taslimu waliweza kubomoa jeneza lililokuwa lina mwili wa mwanafunzi wa SUA, Munchari Lyoba na kuchana chana sada kwa imani kwamba kuna mali iliyokuwa imehifadhiwa humo Mwili wa Lyoba alikuwa ukipelekwa Tarime mkoani Mara kuzikwa.

Kabla ya kutolewa kwa hukumu hiyo,Mwendesha Mashitaka Sajenti wa Polisi,Godwel Lawrence amesema pamoja na washitakiwa wote kutokuwa na rekodi yoyote ya makosa ya jinai lakini kitendo walichokifanya ni cha kinyama na cha aibu mbele ya macho ya jamii.

 “Kwa hiyo,Mheshimiwa hakimu naiomba mahakama yako tukufu iwape washitakiwa wote adhabu kali ambayo itakuwa fundisho kwao na watu wengine wanaotarajiwa kufanya makosa ya jinai kwa kutumia silaha au nguvu ya aina yoyote”,amesema Lawrence.

Kwa upande wao washitakiwa kila mmoja kwa nafasi yake walitoa maombolezo yaliyofafana kwamba wana familia zinazowatengea kwa asilimia kubwa na kwamba kosa hilo ni la kwanza kutenda toka wazaliwe Hivyo wakaiomba mahakama hiyo iwape adhabu nafuu.

 Akisoma hukumu hiyo iliyochukua  saa moja na dakika 45,Hakimu Mfawidhi wa Mahakama ya Wilaya ya Singida,Flora Ndale amesema ushahidi wa upande wa mashitaka umethibitisha bila kuacha chembe chembe ya shaka kwamba washitakiwa wana hatia kama walivyoshitakiwa.

 “Walalamikaji wote ambao walikuwa abiria kwenye gari lililokuwa likisafirisaha mwili wa marehemu mwanafunzi wa SUA maelezo yao yanafafana wote waliweza kuwatambua vema washitakiwa kwa msaada wa taa za gari na mbalamwezi”,amesema.

Ndale amesema kiongozi wa msafara huo Makaranga Nona,aliiambia mahakama kwamba mshitakiwa wa pili na wa tatu walimwamuru kufungua ‘brief case’ mbele ya gari huku mwanga wa taa za gari ukiwamulika.

 “Kama hiyo haitoshi,dereva wa gari hilo Kalistus Malipula ameiambia mahakama hii kwamba
mshitakiwa wanne alimbebeleza kwa muda mrefu ampe simu mbili za marehemu na maombi hayo alikuwa akiyatoa huku mwanga wa taa za gari ukimmulika”.


 Kwa mujibu wa Mwendesha Mashitaka Lawrence washitakiwa hao wametenda kosa hilo Desemba sita mwaka jana saa saba usiku huko katika barabara kuu ya Dodoma – Singida eneo la kijiji cha Kisaki.

BOFYA HAPA KUSOMA HABARI YA KUPORWA NA KUSACHIWA MAITI

No comments:

Post a Comment