Tuesday, October 22, 2013

Watoto waninginizwa kichwa chini miguu juu huku wakila bakora za nguvu baada ya kulamba sukari.

Kamanda wa jeshi la polisi mkoa wa Singida, ACP Geofrey Kamwela akitoa taarifa ya kushikiliwa kwa mkazi wa kijiji cha Mgongo wilaya ya Iramba Joyce Isaya (30) kwa tuhuma ya kuwafanyia ukatili wa hali ya juu watoto wa kambo kwa madia ya kulamba sukari na kukomba mboga aina ya Mlenda. Mtuhumiwa anadaiwa kuwaning’iniza kwa kamba ya katani kwenye dari watoto hao miguu juu na vichwa chini na kisha kuanza kuwachapa viboko sehemu mbalimbali za miili yao.

Jeshi la Polisi Mkoa wa Singida linamshikilia Joyce Isaya (30) mkazi wa kijiji cha Mgongo tarafa ya Shelui wilaya ya Iramba kwa tuhuma ya kuwafanyia ukatili wa hali ya juu watoto wawili.

Mtuhumiwa huyo inadaiwa kuwafunga kamba ya katani miguuni na kuwaning’iniza kwenye dari miguu juu vichwa chini na kuwachapa viboko katika sehemu mbalimbali za miili yao.

Watoto hao ambao ni wa kambo (majina yao tunayo),mmoja ana umri wa miaka 10 na mwingine 8. Inadaiwa kupewa adhabu hiyo kwa madai kuwa walilamba sukari na kukomba mboga yoye aina ya mlenda.

Kamanda wa Jeshi la Polisi Mkoa wa Singida,ACP,Geofrey Kamwela, amesema tukio hilo la kusikitisha na la ukatili wa hali ya juu,limetokea oktoba 16 mwaka huu saa 9.30 alasiri huko katika kijiji cha Mgongo.

Akifafanua,amesema siku ya tukio majirani walisikia vilio vikali kutoka kwa watoto hao ambao walikuwa wamefungiwa kwenye chumba cha nyumba yao na mama yao wa kambo huku wakichapwa viboko.

“Baada ya majirani hao kufanya uchunguzi ndipo walipowaona watoto hao wamening’inia kwenye dari miguu juu vichwa chini na mama yao huyo wa kambo akiendelea kuwachapa viboko kwenye miili yao.

Baada ya kuona kitendo hicho cha kikatili, majirani hao haraka
walitoa taarifa polisi na polisi walifika haraka wakakuta mama huyo akiendelea na ukatili wake”, amefafanua.

Kamwela amesema wakati mtuhumiwa akifanya unyama huo,mume wake Waziri Willson (33) alienda maeneo  ya Sekenke kwa ajili ya kuchimba dhahabu.

“Chanzo cha watoto hao kuchapwa ni kudaiwa kuiba sukari pamoja na kukomba mboga yote. Upelelezi ukikamilika mtuhumiwa atafikishwa mahakamani kujibu shitaka linalomkabili”, amesema kamanda Kamwela.


Wakati huo huo, Septemba 25 mwaka huu Zuhura Fred (6) aliyekuwa mkazi wa New Kiomboi mjini wilayani Iramba alifariki dunia baada ya kumwangiwa maji yaliyokuwa yatumike kupikia ugali. Alimwagiwa maji hayo baada ya kuchelewa kuleta mwiko wa kupikia ugali.Habari zaidi Bofya Hapa

No comments:

Post a Comment