Tuesday, March 5, 2013

Diwani wa Unyamikumbi Singida ataka watendaji wa halmashauri kusimamia kikamilifu misaada inayotolewa na Mh. Dewji.

Diwani wa kata ya Unyamikumbi Mosses Shaban Ikaku, akizungumza kwenye kikao cha baraza la madiwani wa manispaa ya Singid. Kikao hicho kilikuwa maalum kwa ajili ya kupitisha bajeti ya manispaa ya Singida kwa mwaka wa fedha wa 2013/2014.

Watendaji wa halmashauri ya manispaa ya Singida wameshauriwa kujenga utamaduni wa kusimamia kikamilifu misaada mbalimbali inayotolewa na mbunge wa jimbo la Singida mjini Mh. Mohammed Dewji, ikiwemo ya sekta ya kilimo ili manispaa hiyo iweze kupaa kimaendeleo.
Rai hiyo imetolewa na diwani (CCM) kata ya Unyamikumbi Moses Shaban Ikaku, wakati akizungumza kwenye kikao maalum cha madiwani ambacho kilipitisha bajeti ya manispaa ya Singida kwa kipindi cha 2013/2014.
Amesema misaada mingi na mikubwa inayotolewa na mbunge Dewji yenye lengo la kuwapatia wananchi maendeleo endelevu, haijafikia malengo yanayokusudiwa.
Moses amesema kwa utafiti na uzoefu wake, miradi hiyo imekuwa haitoi matunda mazuri kutokana na sababu kuu moja, nayo ni watendaji/wataalam kutoisimamia kikamilifu.
 Diwani huyo meisema mfano hai na mzuri, ni wa msaada wa hivi karibuni wa majembe ya kukokotwa na ng’ombe zaidi ya 500 na zaidi ya tani 60 za mbegu bora za dengu, choroko na mbaazi.
Moses amesema msaada huo wenye thamani kubwa na ambao ulikuwa na sharti nafuu ambalo ni wakulima 10 kujiunga kwenye kikundi, kama ungesimamiwa kikamilifu na wataalam wa kilimo na watendaji wengine, ungewakomboa kiuchumi wakazi wa jimbo la Singida mjini.
Aidha, amesema endapo majembe hayo yangetumika ipasavyo, ingechangia wakulima kulima kisasa na kupanua ukubwa wa mashamba yao, kitendo ambacho kigesaidia wakulima kupata mapato makubwa na kupelekea kununua trekta kubwa.
“Nachukua fursa hii kumshukuru na kumpongeza mbuge wangu Mh. Dewji , kwa kugawa majembe zaidi ya 500 ya kukokotwa na wanyama kazi, lengo lake ni zuri mno, kwa sababu analenga kusaidiana na serikali katika kufikia malengo ya kilimo kwanza. Lakini nasikitika sana, kusema msaada huu huenda usizae matunda mazuri kwa sababu hausimamiwi kikamilifu na wataalam wa kilimo na watendaji wengine”amesema Moses kwa masikitiko.
Amesema msaada huo na mingine mingi inayotolewa na Mh. Dewji, imekuwa kama ni kiini macho mbele ya wataalam na watendaji wa manispaa, na kwa sababu hiyo, imekuwa haifikii lengo.
Moses amesema wakilitambua hilo na wakasimamia misaada inayotolewa kwa wananchi ipasavyo, misaada hiyo itakuwa na tija zaidi kwa maana kwamba itasaidia kupaisha maendeleo ya wananchi.
Pia kwa njia hiyo, itamvutia zaidi mbunge Dewji na wadau wengine kuongeza misaada zaidi ambayo itawakwamua wananchi kutoka kwenye lindi la umaskini.

No comments:

Post a Comment