Saturday, March 30, 2013

umuhimu wa walemavu kushirikishwa kikamilifu katika uundaji wa mabaraza ya katiba.

 Bango la shule ya msingi mchanganyiko Ikungi wilaya ya Ikungi mkoa wa Singida.

Baadhi ya wanafunzi wa shule ya msingi mchanganyiko Ikungi,wakiwa darasani.
Mwalimu mkuu wa shule ya msingi mchanganyiko Ikungi wilaya ya Ikungi Olivary Kamilly akizungumza na waandishi wa habari (hawapo kwenywe picha) juu ya umuhimu wa walemavu kushirikishwa kikamilifu katika uundaji wa mabaraza ya katiba.


Mwalimu mkuu wa shule ya msingi mchanganyiko wilaya ya Ikungi mkoa wa Singida Olivary Kamilly, amependekeza walemavu washirikishwe kikamilifu katika mabaraza ya katiba kwa madai kuwa ndio wenye uwezo mzuri wa kuwakilisha mahitaji yao.
Mwalimu Kamilly mwenye taaluma ya ufundishaji walemavu, ametoa pendekezo hilo wakati akizungumza na Singida Yetu Blog ofisini kwake, juu ya uundaji wa mabaraza ya katiba.
Amesema mahitaji ya walemavu yataelezwa vizuri zaidi na walemavu wenyewe kwa kuwa wanaishi na ulemavu.
Akifafanua  zaidi, mwalimu huyo mkuu amesema
sifa hiyo ya kuyajua kwa undani mahitaji ya walemavu, hata mtaalamu yeyote wa watu wenye ulemavu au mtu yeyote ambaye si mlemavu, hawezi kuwa na sifa ya kuyafahamu mahitaji yote ya mlemavu.
Katika hatua nyingine, mwalimu Kamilly amependekeza katiba ijayo ionyeshe wazi nini kifanyike ili kuonyesha thamani ya utu wa watu wenye ulemavu.
Aidha, amesema katiba ijayo itamke wazi nini kifanyike kwa wazazi/walezi wenye tabia ya kuwaficha watoto wao wenye ulemavu badala ya kuwapeleka shule.
Mwalimu Kamilly amesema katiba ya sasa ibara ya 12 kifungu 1-2, kinasema kuwa binadamu wote huzaliwa huru na wote ni sawa pia kila mtu anastahili heshima ya kutambuliwa na kuthaminiwa utu wake.
Hata hivyo, amesema ibara hiyo ipo kinadharia zaidi kuliko kiutendaji, kwani walemavu wengi wanadharauliwa, wananyanyaswa na wanaonekana ni mzigo katika jamii.
Shule ya msingi mchanganyiko Ikungi mbali ya kuwa na wanafunzi wasio na ulemavu, pia ina wanafunzi walio na mahitaji muhimu ambao ni wasioona 42, uoni hafifu 19, ulemavu wa ngozi (albino) 15 na ulemavu wa viungo watano.

No comments:

Post a Comment