Wednesday, October 30, 2013

Diwani wa Chadema kizimbani kwa kuvunja ofisi ya kijiji na kuiba.

Diwani wa CHADEMA kata ya Iseke jimbo la Singida magharibi Emmanuel Jackson Jingu (45) akiwa kwenye chumba cha mahakama ya hakimu mkazi mjini Singida, akisubiri kusomewa kesi yake ya kuvunja na kuiba kwenye ofisi ya serikali ya kijiji cha Nkhoiree.Diwani Emmanuel alishinda nafasi hiyo hivi karibuni kwenye chaguzi ndogo zilizofanyika hivi karibuni.

Diwani wa Kata ya Iseke Tarafa ya Ihanja (CHADEMA) Jimbo la Singida Magharibi, Emmanuel Jackson Jingu (45) amepandishwa kizimbani katika Mahakama ya Hakimu Mkazi mjini Singida akikabiliwa na mashitaka mawili ya kuvunja ofisi ya kijiji cha Nkhoiree.

Mapema Mwendesha Mashitaka Mwanasheria wa Serikali, Petrida Muta alidai mbele ya Hakimu Asha Mwetindwa kuwa mnamo septemba 20 mwaka huu saa 8.30 mchana mshitakiwa alivunja nyumba kwa lengo la kuiba mali huku akijua wazi kwamba kitendo hicho ni kinyume cha sheria.

Mwendesha Mashitaka Muta alimsomea mshitakiwa shitaka la pili kuwa siku hio hiyo na wakati huo huo mshitakiwa baada ya kuvunja mlango wa nyumba inayotumiwa na serikali ya kijiji cha Nkhoiree aliweza kuiba vifaa mbalimbali vyenye thamani vya thamani ya shilingi 298,000.

Alitaja vifaa hivyo na thamani yake kwenye mabano kuwa ni vocha (hazikuweza kuelezwa ni za nini)(32,000),vitabu vya risiti (12,000),cash book (10,000),risiti za ushuru (28,000),hati za malipo (4,000),vitabu vya ushuru (10,000),risiti za zahanati (28,000) na madumu tupu 100 (150,000).

Mshitakiwa alikana mashitaka hayo na ameenda rumande baada ya kukosa mdhamini wa ahadi ya shilingi
500,000 na mali isiyohamishika. Kesi hiyo ambayo imetajwa kwa mara ya kwanza jana inatarajiwa kutajwa tena Novemba 11 mwaka huu.


Diwani Jingu ameshinda nafasi hiyo hivi karibuni baada ya kuigaragaza CCM kwenye uchaguzi mdogo iliofanyika hivi karibuni.

No comments:

Post a Comment