Saturday, January 12, 2013

Manispaa ya Singida yafanikiwa kupanda miti zaidi ya milioni 2.6 katika kipindi cha miaka minne.

 Mkuu wa wilaya ya Singida mwalimu Queen Mlozi,akishiriki kupanda miti katika siku ya uzinduzi wa upandaji miti katika manispaa ya Singida.
Mkuu wa wilaya ya Singida mwalimu Queen Mlozi akizungumza na wananchi waliohudhuria uzinduzi wa  siku ya upandaji miti katika manispaa ya Singida.Uzinduzi huo ulifanyika katika shule ya msingi na Unyinga kata ya Mandewa.

Halmashauri  ya manispaa ya Singida imepanda miti 2,645,314 ya aina mbalimbali katika kipindi cha miaka minne iliyopita.
Akitoa taarifa yake fupi siku ya uzinduzi wa upandaji miti katika manispaa hiyo, Mkurugenzi wa manispaa ya Singida Mathias Mwangu amesema zoezi la upandaji miti katika manispaa hiyo, lengo lake ni kuzuia mmomonyoko wa ardhi na kudhibiti kuenea kwa
jangwa na kufanikisha upatikanaji wa kivuli, matunda, kuni na mbao.
Ametaja faida zingine kuwa ni kuhifadhi na kutunza vyanzo vya maji na kupendezesha mji na kuweka mandhari nzuri.
Mwangu amesema ili kufanikisha na kuhamasisha upandaji miti kwa kuongeza uzalishaji wa miche ya miti, wakuu wa idara 13 wa manispaa, wameotesha miche ya miti 13,000 ya aina mbalimbali.
Miche hiyo imeoteshwa kwenye kitalu kilichopo kwenye eneo la ofisi kuu.
Aidha, Mkurugenzi huyo amesema manispaa  imetenga jumla ya shilingi 3,200,000 kwa ajili ya kuotesha miche zaidi ya 15,000 kwenye kata za Mwankoko, Uhamaka, Mtipa na Mandewa.
Naye mgeni rasmi katika uzinduzi huo, Mkuu wa wilaya ya Singida Mwalimu Queen Mlozi amezitaka mamlaka zinazohusika zikiwemo serikali za vijiji, zihakikishe zinakomesha tabia ya uvunaji ovyo wa miti.
Mlozi amesema haya malori kutoka mikoa ya Manyara na Arusha yanayokuja kubeba mkaa wetu, yakamatwe na sheria za mazingira zitumike katika kuhakikisha hawafanyi  biashara ya mkaa kutoka wilaya ya Singida.

No comments:

Post a Comment