Saturday, January 12, 2013

Wakazi wa Singida wenye maradhi yanayohitaji upasuaji kupatiwa tiba na madaktari bingwa kutoka Marekani.

                                   Jengo la hospitali ya mkoa lililopo Singida mjini.

Madaktari bingwa 26 kutoka Marekani wataendesha zoezi maalumu la utoaji tiba kwa wagonjwa wenye maradhi yanayohitaji upasuaji, utakaofanyika katika hospitali ya mkoa wa Singida.
Akiongea na Singida Yetu Blog, Mganga mfawidhi hospitali ya mkoa Singida Dkt. Suleiman Muttan amesema huduma hiyo ni mpango wa kila mwaka wa Shirika la Outriach International kutoa huduma hiyo Singida.
Dkt. Muttan amesema, kati ya wataalamu mbalimbali wanaokuja, watakuwepo pia madaktari bingwa wa
upasuaji kwa watoto na magonjwa ya wanawake.
Amesema watakuwa na kazi ya kuchunguza wagonjwa ambao tayari wameanza kujiorodhesha katika hospitali hiyo.
Mganga huyo wa mkoa amesema kuwa, madaktari hao watachunguza wagonjwa wote, ili kubaini wanaohitaji upasuaji na wale wanaostahili kupata huduma ya uvimbe bila kupasuliwa.
Amebainisha kuwa, tayari wagonjwa wengi wameanza kujitokeza na kujisajili, kwa ajili ya kunufaika na huduma za upasuaji kutoka kwa madaktari bingwa hao.
Naye mwenyeji wa wataalamu hao hapa nchini, Rais wa shirika hilo upande wa Afrika, ‘Outriach Africa’, Mike Kitwaka amesema timu hiyo ya madaktari itatoa huduma kwa muda wa wiki mbili, kabla ya kurejea Marekani.
Amesema kundi la mwanzo la watu 26 ni moja kati ya timu tatu zitakazowasili mwaka huu kutoa tiba, Kundi la pili litakalokuja baadaye litakuwa na watu 50 na kundi la mwisho zaidi ya watu 36 litamalizia baadaye kuja kutekeleza kazi mbalimbali za shirika hilo.
Shirika hilo limekuwa likileta wataalamu hao kila mwaka na mwaka jana madaktari bingwa 43 kutoka nchini Marekani walikuja nchini na kutoa huduma za tiba katika hospitali ya mkoa wa Singida.

No comments:

Post a Comment