Thursday, January 3, 2013

Viongozi ngazi mbalimbali Singida watakiwa kuhakikisha wananchi hasa wa vijijini wanakuwa na uelewa wa haki zao za msingi.

 Mkuu wa wilaya ya Singida Mwalimu Queen Mlozi akizungumza kwenye ufunguzi wa mdahalo uliohusu uimarishaji wa mahusiano kati ya wananchi, wabunge, madiwani na watendaji wa serikali.Mdahalo huo uliandaliwa na shirika lisilo la kisereikali la SINGONET.
 Mratibu wa SINGONET Maendeleo Makoye,akitoa taarifa yake mbele ya mdahalo uliohusu uimarishaji wa mahusiano kati ya wananchi,wabunge na watendaji wa serikali uliofanyika mjini Singida.
Baadhi ya wadau wa maendeleo wa mkoa wa Singida waliohudhuria mdahalo maalum uliohusu uimarishwaji wa mawasiliano kati ya wananchi,wabunge, madiwani na watendaji wa serikali.Mdahalo huo uliofanyika kwenye ukumbi wa mikutano wa kanisa katoliki mjini Singida, uliandaliwa na shirika la SINGONET.

 Mkuu wa Wilaya ya Singida  Mwalimu Queen Mlozi amewaagiza viongozi wa ngazi mbalimbali wakiwemo wa mashirika yasiyo ya kiserikali ( NGos), kuongeza kasi ya kuhakikisha kila mwananchi na hasa wa
vijijini, wanakuwa na uelewa mpana  wa haki zao za msingi.
Mlozi ametoa agizo hilo wakati akifungua mdahalo wa kuimarisha mahusiano ya wananchi na wabunge wao na watendaji wa serikali, ambapoa amesema serikali pekee haiwezi kufanya kazi zote za kuwaletea maendeleo wananchi pamoja na kuwaelimisha juu ya haki zao za msingi.
Akifafanua zaidi Mlozi amesema kuwa wananchi wakifahamu haki zao za msingi, pamoja na kwamba hawatadhulumiwa, hali hiyo itachochea ari ya kushiriki kujiletea maendeleo endelevu.
Aidha, amesema maendeleo ya kweli ya wilaya ya Singida na mkoa kwa ujumla, yataletwa na wananchi wenyewe, serikali wajibu wake ni kuhamasisha na kushirikiana na wananchi katika kufikia malengo..
Kuhusu wananchi, amesema wajibu wao ni kushirikiana kwa karibu na serikali yao  na kuhudhuria bila kukosa mikutano ya maendeleo ili kupata maelekezo muhimu na  ushauri wa kitaalamu kwa ajili ya kutatua kero zao.
Wakati huo huo, mkuu huyo wa Wilaya ameipongeza asasi ya SINGONET, kwa juhudi zake za kusaidiana na serikali kufika kuhamasisha ushiriki wa pamoja wa wananchi katika kubuni, kupanga na kutekeleza mpango ya maendeleo yao.
Mdahalo huo uliohudhuriwa na wadau zaidi ya mia mbili, uliandaliwa na SINGONET na kufadhiliwa na The foundation for civil society.

No comments:

Post a Comment