Friday, January 4, 2013

Wazazi manispaa ya Singida watakiwa kujenga utamaduni wa kuzungumza na watoto wao juu ya Ukimwi na namna ya kujikinga.

 Mkufunzi wa mafunzo juu ya UKIMWI na namna bora ya kujikinga na maambukizi ya virusi vinavyosababisha ugonjwa hatari wa UKIMWI, Dk. Elia Petro akiwajibika darasani.
 Baadhi ya wanafunzi wa shule za msingi na sekondari katika manispaa ya Singida,wanaohudhuria mafunzo juu ya madhara yatokanayo na UKIMWI.Mafunzo hayo yanaendeshwa na Kituo cha vijana cha mjini Singida,kinachomilikiwa na kanisa la Pentekoste (FPCT).
Kituo cha vijana mjini Singida kinachomilikiwa na kanisa la Pentekoste (FPCT) mjini Singida.

Jumla ya wanafunzi zaidi ya 100 wa shule za msingi na sekondari katika manispaa ya Singida, wanahudhuria mafunzo juu ya UKIMWI na namna bora ya kujikinga na ugonjwa huo hatari ambao hadi sasa, hauna kinga wala chanjo.
Wanafunzi hao kwa sasa wapo mapumziko hadi Januari shule zitakapofunguliwa.
Mafunzo hayo yanatolewa na kituo cha vijana Singida kinachomilkiwa na kanisa la Pentekoste (FPCT) la mjini Singida.
Mratibu wa mafunzo hayo Peter Samweli, amesema wanafunzi hao ni wale wenye umri wa miaka 12 hadi 15, na awamu ya kwanza ya mafunzo hayo, yalihudhuriwa na wanafunzi  60.
Amesema awamu ya pili inayoendelea hivi sasa, ina wanafunzi 40 ambao pamoja na kujifunza juu ya UKIMWI wenyewe, pia wanafundishwa namna bora ya kujikinga na ugonjwa huo.
Peter amesema vile vile wanafundishwa juu ya athari za madawa ya kulevya, ulevi na namna nzuri ya kujikinga na mimba za utotoni.
Katika hatua nyingine, Peter ametoa wito kwa wazazi na walezi, kujenga utamaduni wa kuzungumza na watoto wao, mara kwa mara juu ya ugonjwa wa UKIMWI na namna nzuri ya kujikinga.
Amewataka wahakikishe watoto wao wanakuwa na ufahamu mkubwa wa athari za UKIMWI, madawa ya kulevya, mimba za utotoni na ulevi, ili waweze kujikinga na mambo hayo ambayo ni hatari kwa maisha yao.

No comments:

Post a Comment