Thursday, January 10, 2013

Shule za sekondari Singida zatakiwa kuwa na maabara tatu zilizokamilika kabla ya Novemba 2013.

 Mkuu wa wilaya ya Singida mwalimu Queen Mlozi (wa pili kushoto) akikagua ujenzi wa maabara tatu za shule ya sekondari kata ya Mitunduruni  jimbo la Singida mjini.Wa kwanza kushoto ni diwani wa kata ya Mitunduruni,Sorongai Pantaleo.
 Diwani wa kata ya Mitundurinu (CCM) jimbo la Singida mjini,Sorongai Pantaleo (wa kwanza kushoto) akizungumza na mkuu wa wilaya ya Singida mwalimu Queen Mlozi ofisini kwa mkuu wa shule ya sekondari kata ya Mitunduruni.
 Mkuu wa wilaya ya Singida,mwalimu Queen Mlozi, (wa pili kutoka kulia) akikagua ujenzi wa choo katika shule ya msingi ya Unkyankindi kata ya Mitunduruni.Wa kwanza kulia ni diwani wa kata ya Mitunduruni Bw.Sorongai Pantaleo.
Baadhi ya vyumba vya madarasa  vilivyojengwa na mbunge wa jimbo la Singida mjini,Mohammed Gullam Dewji.
  
Mkuu wa wilaya ya Singida Mwalimu Queen Mlozi amewahimiza wakuu wa shule za sekondari kuwa wabunifu katika kutafuta misaada na fedha kwa ajili ya kugharamia ujenzi  wa maabara.
Amesema kwa vile sio rahisi kwa serikali kufanya kila kitu ikiwemo kujenga kwa mpigo maabara katika shule zote za sekondari nchini, kuna umuhimu mkubwa kwa wananchi na wadau wengine kusaidiana na serikali.
Mkuu huyo wa wilaya ametoa changamoto hiyo wakati akizungumza na
kamati ya ujenzi wa maabara ya shule ya sekondari ya kata ya Mitunduruni jimbo la Singida mjini.
Amesema wakuu wa shue za sekondari  ni lazima watambue kuwa wanalo jukumu la kuhakikisha shule zao zinakuwa na maabara tatu zilizokamilika kabla ya Novemba mwaka huu.
Mkuu huyo wa wilaya amewataka waache tabia ya kukaa tu ofisini na badala yake wachakarike kutafuta ufadhili mbalimbali ikiwemo kwenye taasisi  zikiwemo za mabenki, mashirika yasiyo ya kiserikali, wafanyabiashara na wadau.
“Njooni ofisini kwangu nitawapa vibali vya kuwaruhusu kuchangisha michango.Wakati wa kuchangisha ni lazima muwe na risiti halali ambazo mtawapa wale wanaowachangia”,alisema Mlozi.
Amesema  kamati za ujenzi  ni lazima zihakikishe zinatoa taarifa za michango kwa wananchi ili waweze kujua fedha zao zilivyotumika.
Aidha Mlozi amesema kamati za ujenzi wa maabara zinapaswa kuhakikisha ujenzi wa maabara unakaguliwa mara kwa mara na mhandisi wa manispaa.
Mkuu huyo wa wilaya katika siku yake ya kwanza alitembelea kamati za ujenzi wa maabara za shule za sekondari tisa na kumaliza ziara yake kwa kutembelea shule nane za sekondari jimbo la Singida mjini.

No comments:

Post a Comment