Wednesday, January 16, 2013

Wakazi wa Iramba watakiwa kulinda misitu.

 Mkuu wa wilaya ya Iramba mkoa wa Singida,Yahaya Nawanda akizungumza kwenye kilele cha siku ya upandaji miti kitaifa wilayani Iramba uliofanyika katika kijiji cha Mbelekese kata ya Ndago.Kushoto (aliyekaa) ni mkurugenzi mtendaji wa halmashauri ya wilaya ya Iramba,Christina Midelo.
 Mkuu wa wilaya ya Iramba Yahaya Nawanda akishiriki kupanda miti katika siku ya upandaji miti kitaifa iliyofanyika kiwilaya katika kijiji cha Mbelekese.
 Maafisa wa maliasili na utalii kanda ya kati, Muze Kajiru (katikati) mtaalamu wa nyuki na mazingira,William Kaaya (kushoto)mtaalamu wa misitu na mazingira na Zakaria Matavi (kulia) mtaalamu wa misitu wakishiriki kupanda miti katika siku ya kupanda miti ya wilaya ya Iramba.
Mkuu wa wilaya ya Iramba Yahaya Nawanda (wa tano kutoka kushoto) akipokea miche ya miti mbalimbali elfu moja  iliyotolewa na ofisi ya malialisi na utalii kanda ya kati.Nawanda alikabidhiwa na Muze Kajiru mtaalamu wa nyuki na mazinmgira kanda ya kati.

Mkuu wa Wilaya ya Iramba mkoani Singida, Yahaya Nawanda ameagiza kila mkazi wa wilaya hiyo kuwa mlinzi wa misitu ili kulinda maliasli hiyo ambayo ni uhai wa viumbe vyote hai inayokabiliwa na tishio la kutoweka.
Nawanda aliyasema hayo jana wakati akizungumza kwenye kilele cha siku ya  upandaji miti wilayani humo  uliofanyika kwenye kijiji cha Mbelekese kata ya Ndago jimbo la Iramba magharibi.
Alisema uvunaji ovyo wa miti katika wilaya hiyo,umesababisha madhara mengi ikiwemo ukame mkali,uhaba wa mvua na
unatishia wilaya hiyo kugeuka kuwa jangwa.
Alisema kila mkazi wa wilaya hiyo ni shahidi mzuri wa madhara makubwa yatokanayo na uvunaji huo usikuwa na uwiano na upandaji miti.
 “Kwa hiyo mimi kama mkuu wa wilaya hii,sikubaliani kabisa na uvunaji huu.Kuanzia sasa ni marufuku mtu kukata mti.Kama mtu anataka kuni,akate matawi na si kuagusha mti mzima.Kwa hiyo,naagiza kuanzia sasa kila mtu awe ni mlinzi wa miti na akimwona mtu anakata,amzomee”,alisema Nawanda.
Katika hatua nyingine, mkuu huyo wa wilaya,ameagiza pia kuwa suala la kuchangia maendeleo katika wilaya hiyo, ni la kufa na kupona.Mtu ambaye hataki kuchangia maendeleo ahame haraka wilayani humo na kwenda kuishi mahali watu hawachangii maendeleo yao.
“Niseme tu kwamba hata mtu akifariki dunia kama anadaiwa michango ya maendeleo yakiwemo ya sekta ya elimu,asizikwe hadi hapo michango anayodaiwa iwe imelipwa ndio azikwe.We mtu anafariki dunia huku akiwa ameaacha watoto wanne nani awagharamie”,alihoji.
Kuhusu ujenzi wa maabara,Dc Nawanda alisema kuwa kila shule ya sekondari ihakikishe inakamilisha ujenzi wa vyumba vitatu vya maabara kabla ya juni 30 mwaka huu.
Kwa mujibu wa afisa maliasili na utalli wilayani Iramba,jumla ya vijiji 75 vinetenga maeneo kwa ajili ya hifadhi ya misitu ya asili yenye ukubwa wa hekta 25,652,shule 167 zimepanda miti kwenye maeneo yao yenye hekta 757.8,vijiji 28 vina mashamba ya miti yenye hakta 481.5 na taasisi 17 zina mashamba ya misitu hekta 30.

No comments:

Post a Comment